HOTUBA YA MGENI
RASMI, MHE. BALOZI DKT. PINDI HAZARA CHANA (MB) WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA KWENYE UZINDUZI WA KAMPENI YA HUDUMA YA MSAADA
WA KISHERIA YA MAMA SAMIA(MAMA SAMIA
LEGAL AID CAMPAIGN) KATIKA UWANJA WA STENDI
YA ZAMANI- MANISPAA YA SINGIDA
10 JANUARI, 2024
Ninawasalimu kwa Salaam ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Kazi Iendelee
Ndugu
Wananchi na Wageni Waalikwa,
Naomba pia kuchukua fursa hii kipekee kumshukuru Mhe. Mkuu wa Mkoa na Kamati yake yote Ulinzi ya Mkoa wa Singida
kwa kuridhia Kampeni hii ifanyike mkoani
kwako ikiwa ni Mkoa wa Sita tangu izinduliwe na kutekelezwa katika mikoa
mingine ikitanguliwa na mikoa ya Dodoma, Manyara, Shinyanga, Ruvuma na Simiyu. Mkoa
wako umekua bega kwa bega katika
maandalizi ya tukio hili muhimu. Asanteni
sana.
Ndugu Wananchi na Wageni
Waalikwa;
Kampeni ya hii ya Msaada wa Kisheria inatokana na Azma ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania ya kuhakikisha kwamba kila mwananchi anafahamu masuala ya kisheria
ikiwemo haki na wajibu wake na kwamba kila mwananchi anaifikia haki na wasiokuwa
na uwezo wa kumudu gharama za mawakili basi waweze kufikia haki kupitia huduma
za msaada wa kisheria. Kwa muktadha huu, Mhe. Rais ametuelekeza kuhakikisha msaada
wa kisheria unatolewa kwa wananchi wote
hususani kundi la wanyonge na wasiokuwa na uwezo ili kupata haki, usawa, amani
na maendeleo. Kama
mnavyofahamu, nchi yetu imeendelea kupiga hatua kubwa katika utekelezaji wa
Haki za Binadamu na Msaada wa Kisheria nchini;
Hivyo, Mhe. Rais anataka kuendelea kuona kuwa
Tanzania inaendelea kuwa nchi tulivu na yenye amani kwa kuwawezesha Wananchi
sio tu kupata msaada wa kisheria bali kuwaelimisha kuhusu haki zao na wajibu
wao kwa Taifa. Kila mmoja wetu akifahamu vizuri haki zake na wajibu wake, ndipo
nchi yetu itasonga mbele kiuchumi.
Ndugu Wananchi na Wageni Waalikwa,
Wizara ya Katiba na Sheria
ninayoiongoza imepewa dhamana ya
kutekeleza majukumu ya Serikali yanayohusu masuala ya Katiba na Sheria za nchi.
Katika utekelezaji wa majukumu haya, Wizara
imeendelea kuzingatia miongozo mbalimbali ya kisera ya Kitaifa ikiwa ni
pamoja na kuhakikisha kunakuwa na
usawa mbele ya sheria, na kuwa wananchi wanapata haki kwa wakati kupitia vyombo vya haki, wanaishi
bila ya ubaguzi wowote, na wanalindwa na
kupata haki sawa mbele ya sheria.
Ndugu Wananchi na Wageni Waalikwa,
Mwaka 2017 Serikali ilipitisha
Sheria ya Msaada wa Kisheria, Sura ya 21 kwa lengo la kuratibu na kusimamia
shughuli za msaada wa kisheria nchini. Na katika hili, huuduma za msaada wa
kisheria zimeendelea kuimarishwa nchini na wananchi wengi wameendelea kupata
huduma za msaada wa kisheria kwa uhakika. Kupitia Sheria hii, Wizara yangu imewasajili
watoa huduma za msaada wa kisheria takribani 250 na wasaidizi wa kisheria takribani 1800
wamesajiliwa na wanatoa huduma hizi za msaada wa kisheria katika mikoa yote
Tanzania Bara. Hii yote ni kuhakikisha upatikanaji wa huduma za msaada wa
kisheria kwa wakati na kwa ufanisi kwa wananchi hususani katika maeneo ya
pembezoni.
Ndugu Wananchi na Wageni Waalikwa,
Wizara yangu imekuwa
ikishirikiana na wadau mbalimbali kutoka katika taasisi za Serikali na zisizo
za kiserikali katika kuhakikisha mipango na shuguli za msaada wa kisheria
zinabuniwa na kutekelezwa kwa lengo la kuwafikia wananchi wengi. Mipango hii ndio
imetupelekea kuanzishwa kwa Kampeni hii
ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia. Lengo likiwa ni kulinda na kukuza upatikanaji wa haki kwa
wote kupitia huduma ya msaada wa kisheria nchini ambayo ni utekelezaji wa
Katiba yetu ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania hususani ibara ya 8 (1) (b) na Ibara ya 13 (1) zinazoweka msingi wa
haki na usawa na ustawi wa wananchi.
Pamoja na Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, masuala haya ya msaada wa kisheria yapo katika
Ibara ya 231(k) ya Ilani ya Chama
cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025 ambayo imetambua umuhimu wa upatikanaji
haki kwa wananchi na inatuelekeza kuimarisha huduma za msaada wa
kisheria hususan kwa Wanawake na Watoto
katika maeneo yote. Wajibu wa Wizara yangu na kuwa kupitia Kampeni hii, ni
kuhakisha kuwa inakidhi matarajio ya Mhe. Rais kwa kuweka mazingira wezeshi ya
wananchi kupata haki kwa usawa, uzingatiwaji wa haki za binadamu na utawala
bora. Mheshimiwa Rais anataka kuona kuwa Tanzania inaendelea kuwa nchi tulivu na yenye
amani kwa kuwawezesha wananchi, sio tu kupata msaada wa kisheria bali wanaelimishwa
waelimisha kuhusu haki zao na wajibu wao kwa Taifa. Tunaamini kwamba, kila mmoja wetu akifahamu
vizuri haki zake na wajibu wake, ndipo nchi yetu itasonga mbele kiuchumi na
kutuletea maendeleo.
Ndugu Wananchi na Wageni Waalikwa,
Niwathibitishie kuwa, Wizara yangu imejipanga kikamilifu katika kuhakakisha kuwa wananchi wa
Tanzania wananufaika na Mama Samia Legal Aid Campaign na kuhakikisha kuwa inawafikia wananchi wote hapa nchini.Kupitia huduma
hii,
msaada wa kisheria unatolewa bure katika Halmashauri zote za Mkoa wa Singida kuanzia kesho tarehe 11 Januari , 2024 hadi tarehe 19 Januari,
2024. Malengo ni kufikia jumla ya Kata 70 na vijiji 210 vya mkoa wa Singida. Wito wangu kwa Wananchi wote wa Mkoa wa Singida na maeneo jirani kuitumia
vizuri fursa hii kwa kuhakikisha kuwa mnashiriki kikamilifu kwa kupata elimu na huduma za masuala
mbalimbali ya kisheria zitakazotolewa
bure. Aidha, niwasihi viongozi
katika ngazi ya Mkoa, Wilaya, Kata na Vijiji kutoa ushirikiano wa kutosha kwa
wataalamu wetu watakapokuwa katika maeneo yenu, muhamasishe wananchi wajitokeze
kwa wingi kupata huduma hii.
Ndugu wananchi na Wageni waalikwa;
Kama mnavyojua, nchi yetu ni kubwa, na idadi ya wananchi pia ni kubwa kama matokeo ya Sensa yanavyoonyesha kuwa zaidi ya watu milioni 61. Ziko jitihada nyingi sana za Serikali za kulinda na kukuza haki za binadamu zilizofanyika na zinazoendelea kufanyika. Serikali imeweka Mikakati ya Kitaifa ikiwemo ya kutokomeza ukatili wa kijinsia; kuimarisha Ulinzi wa Mtoto na kuweka mifumo ya kisheria ya kulinda haki za wanawake na watoto..
Ndugu wananchi na Wageni waalikwa;
Wote ni mashuda kuwa kwa muda mrefu sasa, vyombo vya habari vimekuwa vikitoa taarifa za unyanyasaji na ukatili wa kutisha dhidi ya wanawake na watoto. Matukio yanayoripotiwa yanaleta tafsiri nyingi; lakini moja la msingi ni umuhimu wa kujenga uelewa wa jamii katika masuala ya haki za binadamu na sheria; kuhamasisha wananchi wote kuzingatia haki na wajibu wao wa kikatiba na wa kisheria katika maisha yao ya kila siku. Aidha, tunatakiwa kulinda watoto wetu dhidi ya ukatili ili tuwe na Taifa lenye staha, maadili na lenye kuheshimu na kuthamini utu wa mtu. Huu ndio urithi tuliopewa na wazee wetu waliotutangulia kuanzia kwenye uongozi wa kitaifa hadi kifamilia, na hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kutimiza wajibu wake na kuzingatia sheria za nchi zilizopo.
Ndugu wananchi na Wageni waalikwa;
Kwa namna ya pekee naomba, nitumie hadhara hii kumshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kwa namna ambavyo anatuongoza kwa kuzingatia Katiba, Sheria na taratibu tulizojiwekea kama nchi. Kila Mtanzania analo jukumu la kusimamia na kuzingatia haki za binadamu, utawala wa sheria, utii wa sheria na elimu ya kikatiba na ya kisheria kwa umma. Haya yote yanafanikiwa kwa uwepo wa sheria zinazotekelezwa, uwepo wa sheria nzuri peke yake hakutoshi, bali pia wananchi wanatakiwa kuelimishwa kuhusu sheria hizo na kuzifahamu, wananchi waelimishwe juu ya masuala ya haki za binadamu ili wafahamu haki na wajibu wao.
Ndugu wananchi na Wageni Waalikwa;
Kwa kuwa Kampeni hii pia
inashiriki katika utatuzi wa migogoro katika ngazi za kijamii, jumla ya migogoro 6,365 iliyohusu masuala ya ardhi, ndoa, mirathi na matunzo ya
watoto ilipokelewa ambapo kati ya hiyo
migogoro 488 ilitatuliwa na
kuhitimishwa katika kipindi cha Kampeni. Migogoro 5,877 inaendelea kushughulikiwa
katika mamlaka mbalimbali za kimahakama
na kiutawala na Wizara kupitia waratibu na wasajili wa mikoa na wilaya imeendelea
kufuatilia utekelezaji wake.
Kampeni hii inawezesha pia huduma
za usajili wa matukio mbalimbali ikiwemo usajli wa vyeti wa kuzaliwa na vifo
kupitia Ofisi ya Kabidhi Mkuu RITA. Jumla wananchi 2,055 (Wanaume1,035 Wanawake
1,020) walisajiliwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa kupitia Ofisi ya
Kabidhi Wasii Mkuu – RITA katika mikoa hii mitano. Kwa upande wa maeneo ya vizuizi,
Kampeni pia iliweza kufikia Vituo vya Polisi 22 na Magereza 17
yametembelewa na huduma kutolewa na katika hili jumla ya Wafungwa na Mahabusu 4,763
wamefikiwa na kupatiwa elimu na huduma
mbalimbali za kisheria.
Ndugu wananchi na wageni waalikwa
Kabla ya kuhitimisha hotuba yangu naomba kutoa
wito kama ifuatayo:
Kwanza; Naomba niwapongeze na kutoa wito kwa viongozi
wote wa dini hapa nchini, bila shaka kwa nyakati tofauti tofauti, viongozi wetu
wa dini wamekuwa wakikemea vitendo vya
uvunjifu wa sheria, mmomonyoko wa maadili katika jamii hususan ukatili uliokithiri
dhidi ya wanawake na watoto. Hakika huduma yenu kwa jamii ina nafasi
kubwa sana ya kubadili tabia, mitizamo hasi na kujenga maadili mema. Niwaombe muendeleze jitihada hizi ili kujenga jamii yenye maadili na yenye kumhofia
Mwenyezi Mungu ambapo chanzo chake ni kuheshimu haki za binadamu, kuzilinda
haki hizo na kuzingatia wajibu wetu wa kikatiba na kisheria. Niwathibitishie kuwa Wizara ya Katiba na Sheria iko tayari kushirikiana na
viongozi wa dini kwa namna yoyote ambayo itafaa katika kampeni hii hata kama
itahusisha kutumia majukwaa yao kutoa elimu kwa umma juu ya haki na wajibu wa Kikatiba na Kisheria. Na niwaombe tena
kushiriki kikamilifu kikamilifu wakati wa utekelezaji wa Kampeni ili muweze
kuendelea kujengewa uwezo katika masuala ya kisheria.
Pili,
kwa ndugu zangu wanahabari
na vyombo vya Habari; niwakumbushe kuwa jukumu
kubwa na muhimu katika Kampeni hii, ninawaomba mjipange vyema kama sekta ili
tushirikiane katika kutekeleza suala
hili muhimu kwa mustakabali wa heshima ya nchi na wananchi wetu. Muhakikishe wananchi
wanapata elimu kwa wakati na msaidie kuibua changamoto mbalimbali za wananchi na
kuhakikisha mnafuatilia ufumbuzi wake hadi mwisho.
Tatu, kwa wanasiasa wenzangu, wito wangu
kwenu naomba tujitahidi kutumia uzoefu
na weledi wetu katika kumuunga mkono Kiongozi wetu, Mama yetu, Mlezi wetu na
Mtetezi wa Wananchi kuondoa kadhia ya
ukatili wa kijinsia na uvunjifu wa haki za binadamu katika jamii yetu.
Tunatambua mchango mkubwa ambao unatolewa
katika jamii.
Nne, kipekee niwashukuru sana asasi za kiraia
kwa mchango wenu mkubwa mnaoendelea
kutoa katika katika nyanja mbalimbali
kwa watanzania. Niwathibitishie
kwamba Serikali inatambua mchango wenu na itaendelea kuunga
jitihada zenu, tunaamini kuwa Kampeni hii inaongeza nguvu katika jitihada zinaendelea. Niwaombe viongozi wenzangu kutoa
ushirikiano wa kutosha kwa watoa huduma za msaada wa kisheria hususan kwa
Wasaidizi wa Kisheria wanaotoa huduma ya
msaada wa kisheria bure katika maeneo yenu katika ngazi ya Kata, Vijiji na
mitaa.
Tano,
kwa upande wa Jeshi
la Polisi, Ili kuchochea upatikanaji
haki na kwa wakati natoa wito kwa Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Singida, kushughulikia kesi zote za ndoa, mimba za
utotoni na ubakaji ambazo zimekaa muda mrefu katika upepelezi bila
kushughulikiwa kwa kuhakikisha watuhumiwa wanapatikana na wanashughulikiwa ili
kuondoka changamoto ya kutoroka kwa watuhumiwa pindi wanapopewa dhamana ama
wanaposikia wanatafutwa na Jeshi la Polisi.
Kampeni hii inatukumbusha uwajibikaji na usimamizi wa maamuzi yenye
kuleta haki, hivyo niwakumbushe watumishi wote kutojihusishwa na masuala ya
rushwa inayopelekea kudhorotesha upatikanaji haki kwa wakati; na
Mwisho, ingawa sio kwa umuhimu, nimuombe Mhe. Mkuu wa
Mkoa wa Singida kuweka mipango endelevu ya upatikanaji wa huduma za msaada wa
kisheria kwa wananchi katika ngazi za kijamii. Uendelevu wa Huduma hii ndio
utakamilisha adhima yetu ya Kampeni. Kwani bila mipango ya uendelevu wa huduma
Kampeni hii haitakuwa imefikia malengo yake.
Ndugu Wananchi na Wageni Waalikwa,
Napenda
kuhitimisha hotuba yangu kwa kuwashukuru
uongozi na wananchi wa Singida kwa mapokezi mazuri na kutufanya tujisikie tuko
nyumbani. Aidha, kipekee niwashuru wadau wa maendeleo na asasi za kiserikali
waliounga mkono katika kufanikisha shughuli hii.
Niwashukuru sana Vyombo vyetu vya habari, vyombo vya ulinzi na
usalama, viongozi wa dini na kimila na wananchi kwa ujumla. Tunawashuruku sana kwa kutambua umuhimu na kufanikisha shughuli
hii. Tunawashukuru kwa
ukarimu wenu na Mungu aendelee kuwabariki.
Sasa baada ya kusema maneno maneno haya, kwa heshima kubwa niliyopewa naomba kutangaza rasmi kwamba utekelezaji wa Kampeni ya Mama Samia ya Huduma za Msaada wa Sheria “Mama Samia Legal Aid Campaign” Mkoa wa Singida imezinduliwa rasmi .
Asanteni
sana kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment