Wednesday, October 05, 2022

Wakulima Mkoani Singida kunufaika na Ruzuku za pembejeo

Wakulima Mkoani Singida watanufaika na ruzuku ya pembejeo za kilimo ikiwemo mbolea na mbegu bora mpaka kufikia mwaka 2025 ikiwa ni Mkakati wa Serikali kupunguza gharama za uzalishaji wa mazao na kuwawezesha kuongeza mitaji yao.

Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 5.10.2022 na Waziri wa Kilimo Hussein Bashe wakati wa kuzindua  msimu wa kilimo na ugawaji wa mbegu za alizeti  zenye ruzuku  kwa wakulima, Mkutano uliofanyika  katika ukumbi wa Kanisa Katoliki Mjini Singida ambapo amewataka wakulima kuongeza maeneo ya kulima ili waweze kupata faida katika Kilimo chao.

Bashe amesema Kilimo ni biashara hivyo wakulima kulima eka mbili au tatu hawezi kupata faida na pia huduma za ugani zinakuwa hazimfiki kikamilifu kwa sababu za kijografia na mazingira yanayowazunguka.

Aidha amewaagiza wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhamasisha wakulima kulima kilimo cha pamoja (block farm) kwakuwa ndicho kitakachoweza kuwaletea manufaa makubwa.

Hata hivyo Waziri Bashe amezitaka Halmashauri kutoa mikopo kwa wakulima kwa kuwa wanachangia zaidi ya asilimia 80 za mapato ya ndani na kuimarisha usalama wa chakula kwa Taifa na mtu mmoja mmoja.

Hata hivyo ameyataka Makampuni ya mbolea ambayo yamesajiliwa kufanya Biashara hiyo kuhakikisha wanaanza kuuza mbolea kuanzia kesho (6.10.2022) kwa wakulima wa Singida kwa kuwa msimu wa kilimo umeshafunguliwa na wakulima wameshaanza kuandaa mashamba.

Waziri huyo ameagiza mbolea yote Mkoani hapo kuuzwa kwa bei ya ruzuku ambapo zipo zitakazouzwa kwa sh. 70,000 kwa kilo, 60,000 na 50,000 kwa kilo na kuwataka wakulima kujiandikisha kwakuwa vigezo pekee vya kupata mbolea hiyo ni kujisajili kwenye mfumo.

Akiwatoa hofu wakulima wa Mkoa huo Waziri Bashe amesema zipo skimu saba7 ambazo zitafanyiwa ukarabati ambazo zipo Wilaya ya Mkalama Singida DC, Singida Mc, Iramba na Itigi ambazo zitasaidia kuinua kilimo cha umwagiliaji.

Mkuu wa Mkoa  wa Singida Peter Serukamba akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi ambaye ni Waziri wa Kilimo, Mkuu wa Mkoa  wa Singida Peter Serukamba amesema Mkoa umejipanga kuongeza eneo la kilimo ambalo litalimwa na AMCOS wakulima wadogo, mashule na wakulima wakubwa.

Serukamba amesema dhamira ya Mkoa ni kuhakikisha unachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za uagizaji wa mafuta ya kula nje ya nchi na kipato cha wananchi kinaongezeka.

Kwa Upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa mbegu za kilimo ASA Dkt. Sophia Kashenje amesema wamejipanga kugawa mbegu kilo 5000 ambapo kwa sasa msimu huu wataleta kilo 2900.

MATUKIO MBALIMBALI KATIKA PICHA WAKATI WA UZINDUZI 


No comments:

Post a Comment