MKUU wa mkoa wa
Singida, Dkt. Rehema Nchimbi, amewaonya watendaji watakaowajibika kusajili
vizazi kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano wasithubutu kuleta urasimu
wa aina yoyote.
Dkt. Nchimbi ametoa onyo hilo wakati akizindua semina kwa
viongozi wa wilaya na mkoa wa Singida kuhusu mpango wa usajili wa watoto chini
ya miaka mitano (Under five birth registration program), uliofanyika kwenye
ukumbi wa mikutano ofisi ya mkuu wa mkoa.
Amewatahadharisha
wasitangulize mbele masuala ya posho bali watekeleze wajibu wao huo huku
wakitarajia thawabu na zawadi kutoka kwa mwenyezi Mungu.
Amesema usajili huo utasaidia Serikali ya awamu ya Tano
kujipanga vema katika kuwahudumia Watanzania kwamadai Serikali
itakuwa na idadi sahihi ya watanzania.
“Sitaki kabisa kusikia saa za kazi mtendaji hayupo ofisini, ofisi
imefungwa, hakuna karatasi au kompyuta imekorofisha. Urasimu wa aina yoyote ni
lazima utakula kichwa cha mtendaji” Dkt. Nchimbi.
Aidha, Dkt. Nchimbi amewaomba viongozi wa madhehebu ya
dini mbalimbali kutenga muda mfupi kwa ajili ya kuhamasisha waumini wao juu ya
mpango wa usajili wa watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano.
“Kusajili watoto sio dhambi, lengo ni zuri tu, nalo ni kujua
idadi ya watanzania ili Serikali iweze kupanga namna bora ya kuwahudumia” amesema.
Mkuu huyo wa mkoa, amesema semina hiyo ibadilike na kuwa kikao
cha kazi ili iweke mikakati itakayouwezesha mkoa wa Singida kuvuka lengo, na
kusajili watoto zaidi.
Awali kaimu mtendaji mkuu wa wakala wa usajili ufilisi na
udhamini (RITA), Emmy Kalomba Hudson, amesema mpango wa usajili wa watoto wa
umri wa chini ya miaka mitano unatarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia sasa.
Emmy Kalomba Hudson Amesema, lengo la kuandaa semina hiyo ni
kuwapa uelewa wa kina viongozi wote katika ngazi ya mkoa na wilaya, ili waweze
kujua kwa kina mambo yote muhimu yanayohusu mpango huo.
Akiijengea nguvu hoja yake hiyo, Emmy amesema,
usajili huo ni hatua inayomwezesha mwananchi kutambuliwa kwa
kusajiliwa na kupata cheti cha kuzaliwa. Cheti hicho ni kiambatanishi cha
kumwezasha mhusika kupata haki mbalimbali na huduma nyingine nyingi za
kijamii.
Akionyesha imani kwamba mkoa wa Singida utafanya vizuri katika
kutekeleza mradi huo, kaimu mtendaji huyo, amesema mwaka 2016 mkoa wa Njombe
ukiwa chini ya usimamizi wa Dkt. Nchimbi, uliweza kusajili watoto asilimia 99.6
kwa kipindi cha miezi mitatu tu.
MATUKIO KATIKA PICHA
Kaimu Mtendaji Mkuu wa wakala wa usajili ufilisi na udhamini (RITA), Emmy Kalomba Hudson akizungumza.
"Cheti cha kuzaliwa ni msingi wa mafanikio yako"
IMETOLEWA NA;
KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO
OFISI YA MKUU WA MKOA
SINGIDA
No comments:
Post a Comment