Monday, October 03, 2022

Wakulima wa korosho Manyoni waahidiwa kupata mashamba yao Novemba 30, 2022.

 

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba amewaahidi wakulima wa korosho Wilayani Manyoni kukabidhiwa mashamba yao ifikapo Novemba 30 tofauti na hapo ataiburuza Polisi kamati nzima inayoshughulikia usafishaji na ugawaji wa mashamba hayo kwa wakulima.

Ahadi hiyo ameitoa leo katika Mkutano na wakulima uliofanyika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo ambapo wakulima hao waliahidiwa awali kupata mashamba yao October 30 mwaka huu yakiwa yamesafishwa lakini kulingana na changamoto za rasilimali fedha Kamati husika imeeleza kwamba hayakuweza kukamilika.

Serukamba ameitaka Kamati hiyo kuhakikisha zoezi la kukabidhi mashamba hayo kwa wakulima linakamilika kufikia Novemba 30 yakiwa yamesafishwa au kutosafishwa mbali na hapo atahakikisha anawapeleka Polisi na kuwafungulia mashtaka ya uhujumu uchumi.

Aidha RC Serukamba amemtaka Afisa ugani wa eneo la Mradi pamoja na Msimamizi wa mradi huo Adelard  Michael Rweikiza kuondoka muda huo huo kwenda kutatua changamoto ya wakulima waliokuwa na  mashamba yanayomilikiwa na watu wawili.

Kwa upande wao wakulima hao wamemuomba RC Singida  kuwabana watu wanaoleta mzaha katika mashamba hayo ambapo waliolipia fedha za mashamba na usafishaji toka mwaka 2019 na wamekuwa wakipoteza muda na fedha kufuatia zoezi hilo ambalo halioneshi kuleta matunda ya hivi karibuni.

Katika hatua nyingine baadhi ya wakulima wa korosho Wilayani hapo wameiomba Serikali kuangalia swala la uvamizi wa Tembo katika mashamba yao na kufanya uharibifu mkubwa na kuhatarisha maisha wa wakulima.

Wamesema makundi hayo ya Tembo wenye watoto yamekuwa tishio kwa Maisha ya wakulima na kusababisha hasara katika mashamba hayo huku wakilalamikia huduma ya Askari wanyamapori kuwa ndogo kutokana na uchache wao na uhaba wa vitendea kazi, jambo ambalo RC Serukamba amesema Serikali italifanyia kazi huku akiwataka kuhakikisha wanatumia mbinu za asili ikiwemo kuweka uzio, kutumia oil chafu wakati Serikali ikiendelea na utatuzi wa changamoto hiyo.

No comments:

Post a Comment