Tuesday, October 25, 2022

RC Serukamba asaini Mkataba wa Lishe na wa Wakuu wa Wilaya.

 

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba tarehe 24.10.2022  amesaini Mkataba wa Lishe baina yake na Wakuu wa Wilaya ambao nao wamesaini na Wakurugenzi wao ili kutekeleza afua hiyo na kuhakikisha wananchi wanapata Lishe Bora na kuondokana na changamoto ya utapia mlo.

Akiongea na wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi hao wa Halmashauri Serukamba amewataka Wakurugenzi kuhakikisha wanatenga fedha kiasi cha Tsh.1000 kwa kila mtoto kama sehemu ya kuondoa tatizo la utapia mlo katika Mkoa huo.

Aidha amewaeleza viongozi wa Mkoa huo kuhakikisha wanasimamia zoezi la Lishe kwa kuwa huko ndio kuandaa kizazi Bora cha baadae.

"Tusiangale tu miradi ile ambayo matokeo yake ni hapo kwa hapo, hili la watoto kuwa na utapia mlo ni hatari sana kwakuwa tutakuwa na watu ambao hawaweze kufikiri vizuri" RC Serukamba

RC ameeleza kwamba Mkoani hapo vyakula vipo vya kutosha lakini uandaaji pamoja na elimu ya Lishe kwa ujumla bado haijawafikia wananchi.

"Wananchi wengi hapa Singida wanakimbilia matunda kwa ajili ya kuuza, mtu ana ng'ombe na mbuzi anakamua maziwa lakini yeye hanywi anauza, inabidi wataalamu tutoe elimu kwa wenzetu alisema Serukamba.

Hata hivyo amewashauri wataalamu wa afya kuanzisha darasa katika vituo vya Afya na Zahanati litakalofundisha namna ya kuandaa Lishe kwa ajili ya watoto na mama wajawazito.

Serukamba akatumia muda huo kumuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa na wa Wilaya pamoja na watu wa Lishe kuongeza utoaji wa huduma hiyo ili Mkoa utoke kwenye asimia 87 ya sasa na kufikia asilimia 100 mwakani.

No comments:

Post a Comment