Tuesday, December 13, 2016

WAZIRI MKUU AIPONGEZA BAKWATA KUANZISHA KITUO CHA MAARIFA AKIWA MKOANI SINGIDA.




















Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa Kassim akizungunza kwenye kilele cha Baraza la Maulid taifa lililofanyika katika kijiji cha Shelui wilaya ya Iramba Mkoani Singida. Majaliwa amewahakikishia waumini wa madhehebu ya dini mbalimbali kuondoa wasi wasi juu ya matukio ya ugaidi kwakuwa serikali iko macho katika kupambana na tishio lolote la kiusalama ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.



Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zuberi Bin Ally akitoa nasaha zake kwenye kilele cha Baraza la Maulid taifa lililofanyika katika kijiji cha Shelui wilaya ya Iramba Mkoani Singida. Pamoja na mambo mengine Mufti amewataka waumini wa dini ya kiislamu na Watanzania wote kuelekeza nguvu zao katika kufanya shughuli zitakazowaingizia kipato.


Baadhi ya waumini wa wilaya ya Iramba na Mkoa wa Singida kwa ujumla waliohudhuria Baraza la Maulid taifa lililofanyika katika kijiji cha Shelui wilaya ya Iramba.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassimu Majaliwa, amepongeza BAKWATA kwa hatua yake ya kuanzisha kituo cha DAARUL MAARIF (nyumba ya maarifa ) kwa ajili ya vijana wa kiislamu kufundishwa elimu ya dini ya ile ya kawaida, ili kuwafanya wawe waislamu bora na raia wema nchini.

Waziri mkuu ametoa pongezi hizo, juzi wakati akizungumza kwenye kilele cha Baraza la Maulid yaliyofanyika kitaifa katika kijiji cha Shelui, wilaya ya Iramba mkoani Singida.

 “Ni matumaini yangu kuwa chombo hicho ambacho mnapanga kukianzisha nchi nzima, kiendeshwe kitaalamu na kwa ualedi wa hali ya juu. Lengo ni kiwe endelevu na pia kifundishe stadi za kazi ambazo zitawasaidia vijana wa kiislamu kujikwamua kutoka kundi la umaskini”,alisema.

Aidha, aliangiza chombo hicho kitumiwe vizuri kuaanda vijana wawe makini na wenye maono na busara ya kuwa viongozi bora kwenye taasisi ya BAKWATA  na taifa  kwa ujumla.

 “Fanyeni chombo  hicho kiwe chem Chem ya fikra za kuleta maendeleo, kutetea haki na kupambana na maadui  wa taifa hili yaani umaskini , ujinga, maradhi  na ufisadi”, amesisitiza.

Alisema hana shaka chini ya uongozi wa Mufti Sheikh Abubakar, chombo hicho pia kitaifanya  BAKWATA itoe mchango mkubwa kwa maendeleo ya jamii nzima ya Watanznia kama yanavyofanya mashirika na taasisi za  dini zingine hapa nchini.

Pamoja na pongezi hizo alisema amefarijika sana na maboresho kadhaa yanayoendelea ndani ya BAKWATA ikiwemo uhakiki wa mali ya Baraza.


Awali Sheikh mkuu na Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakari Zeberi bin Ally, alitumia fursa hiyo  kuhimiza  mshikamano miongoni mwa waumini wa madhehebu mbali mbali ya dini,  ili Tanzania iendelee  kubaki kisiwa cha amani na utulivu.

Aidha, amewataka waumini wa kiislamu na wasio waislamu kufanya kazi halali kwa bidii ikiwemo biashara, kilimo na ufugaji ili kujikomboa kiuchumi.
  
Katika hatua nyingine, Mufti alisema katika kipindi hiki  nyumba nyingi hazina darasa la malezi kwa vijana  kama ilivyokuwa miaka ya nyuma,kitendo kinachochochea maadili kuporomoka kwa kasi kubwa.

“Majumba yetu sasa ni matupa hayana darasa la malezi mema. Hatua hiyo imetupeleka pabaya maadili na  heshima imeporomoka. Zamani mtoto akimwona mtu aliyemzidi umri alikuwa anamkimbilia na kumsaidia kubeba mzigo hadi nyumbani kwa mtu huyo. Sasa hivi tabia hiyo njema , imetoweka”,amesisitiza.
  
Akifafanua Mufti Ally, alisema kijana wa sasa anajiona  hana sababu ya kumpokea mzigo mtu aliyemzidi umri, mzee/mtu aliyemzidi umri kijana umri,naye amejawa na hofu kubwa kwamba akimkabidhi kijana mzigo wake mzigo huo, hautakuwa salama”,alisema.

Kwa hali hiyo, alitumia fursa hiyo kuwataka wazazi/walezi kujenga utamaduni wa kutoa malezi bora kwa watoto wao,ili kulijenga taifa lenye watu wanaomwogopa Mungu waadilifu, waaminifu na wazalendo kwa nchi yao.

Picha/taarifa na Gasper Andrew.

No comments:

Post a Comment