Wednesday, April 30, 2014

RAIS MSTAAFU MKAPA ATEMBELEA SINGIDA, AKABIDHI NYUMBA 30.

Rais Mstaafu Mkapa akikata utepe katika moja ya nyumba za watumishi wa Afya wa Zahanati ya Senenemfuru, akishuhudiwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Parseko Kone na Mkuu wa Wilaya ya Singida Mwl. Queen Mlozi.

"Mchakato wa kupata Katiba Mpya vyovyote utakavyoishia Watanzania tuhakikishe tunabaki na Amani, Utulivu, Upendo na Ushirikiano tuliokua nao Miaka hamsini iliyopita".

Rai hiyo imetolewa leo na Rais Mstaafu wa Awamu ya tatu Mh. Benjamin William Mkapa wakati akizindua na kukabidhi nyumba 30 za Watumishi wa Afya za Mkoa wa Singida katika sherehe za makabidhiano zilizofanyika katika Zahanati ya Senene Mfuru, Kata ya Ughandi, Tarafa ya Mtinko wilayani Singida.

Rais Mstaafu Mkapa amesema amekuwa akipata mialiko mingi ya kimataifa kutokana na uzoefu alioupata kwa kuwatumikia wananchi ambao walimwezesha kutimiza wajibu wake vema hivyo haipaswi kuharibu sifa nzuri ya Tanzania kimataifa.

Amesisitiza kwa amani upendo, ushirikiano na utulivu ni tunu ambayo ambazo zimekuwa zikiitambulisha nchi yetu na kuwapongeza wananchi wa Mkoa wa Singida kwa kupenda maendeleo.

Rais Mstaafu  Mkapa ameongeza kuwa ujenzi wa nyumba hizo utasaidia kuboresha huduma za afya kijijini hapo na Mkoa wa Singida.

Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa akifurahia jambo na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Parseko Kone mara baada ya kuzindua nyumba za watumishi wa Afya Mkoani Singida na picha inayofuata ni moja ya nyumba hizo.

Akisoma taarifa ya ujenzi wa nyumba hizo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Benjamin W. Mkapa HIV/AIDS Foundation Dkt. Ellen Senkoro amesema nyumba hizo zimejengwa na taasisi hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa jumla ya zaidi ya shilingi bilioni 1.9.

Dkt. Senkoro amesema kila nyumba imegharimu zaidi ya shilingi milioni 64 ambapo nyumba nane zinatumia umemem wa kawaida na 22 zinatumia umeme wa nishati ya jua.

Amesema nyumba hizo ambazo zimejengwa katika wilaya za Iramba, Manyoni na Singida na kila wilaya kupata nyumba kumi, ni sehemu ya mradi wa taasisi hiyo wa kuimarish mfuo wa Afya katika maeneo ya vijijini, yenye mazingira magumu au yenye mahitaji zaidi.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Benjamin W. Mkapa HIV/AIDS Foundation Dkt. Ellen Senkoro akisoma taarifa ya ujenzi wa nyumba hizo.

Naye Mkuu wa  Mkoa wa Singida Dkt. Parseko Kone amemshukuru Rais Mstaafu Mkapa kwa ujenzi wa nyumba hizona kuongeza kuwa ujenzi wa nyumba hizo unaodhihirisha moyo wa upendo na kujali wa Rais huyo.

Aidha Dkt. Kone amemshukuru rais huyo kwa kuleta maendeleo katika Mkoa wa Singida na kumuomba ushirikiano katika kufanikisha ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida.


Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Parseko Kone akihutubia wananchi wa Senene mfuru.
 
Rais Mstaafu Benjamin Mkapa akiagana na wananchi wa Senene mfuru.

No comments:

Post a Comment