Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe.Halima Dendego ametoa rai kwa wazazi kuhakikisha wanafuatilia vema mienendo ya watoto wao hasa katika sikukuu ya leo ya Eid AL Fitr ambazo watoto huwa na uhuru mwingi wa kutembea peke yao maeneo mbali mbali.
Ameyasema hayo leo katika sala ya asubuhi ya kusherehekea siku kuu ya Eid Al Fitr baada ya kumalizika kwa mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Mhe.Dendego Amesema kuwa katika kipindi cha siku kuu zinazojumuisha watu wengi wa kila rika ni vema watoto wakapatiwa uangalizi maalum kwa lengo la kuwaweka katika mazingira rafiki ikiwemo kutembea pamoja nao badala ya kuwaacha pekee yao,kuwa makini katika vyakula na vinywaji wanavyotumia kwa kuhakikisha ni Salama kiafya pia kulingana na umri wao.
Pia amesisitiza kuwaweka katika mazingira rafiki ili kuepusha kufanyiwa kitendo visivyo vya kimaadili na watu wasiofahamika na kuharibu utu wao kwa lengo la kuwaweka salama na kukua vema kiafya,kimwili, na kiakili.
Sambamba na hilo Mheshimiwa Dendego amewasilisha salamu za Rais Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan kwa waumini wa dini ya kiislamu kwa kuwataka kusherehekea kwa amani na kuyaishi yale yote yaliyofanyika katika mwezi Mtukufu wa Ramadhan kwa kudumisha upendo,amani,kusaidiana na kutembeleana.
"Tusherehekee sikukuu ya leo kwa amani,tutaishi yake yote mema tuliyoyatenda mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa kusaidiana,kutembeleana, na kuwajali wenye mahitaji muhimu,Pia tuwape watoto uangalizi mzuri katika siku kuu kwa kuwapa uangalizi kuhakikisha wapo salama muda wote wa sikukuu na baada ya sikukuu za Eid."amesema Mhe.Dendego.
Awali Sheikh wa Mkoa wa Singida,Sheikh Issa Nassoro,amewashauri waumini wa dini ya kiislamu kuhakikisha wanawapa ushirikiano wa kutosha Viongozi wa Serikali kwa kuwasikilza ,kutii na kufuata maagizo yanayotolewa na Serikali kwa manufaa ya wote.
Amesisitiza kuwa kutowapa ushirikiano Viongozi hao ni chanzo cha mtafaruku na changamoto mbali mbali katika jamii kwani maendeleo hayatakuwapo endapo kukiwa na matabaka kati ya wananchi na viongozi wao mfano kuwepo kwa milipuko ya magonjwa mbalimbali ya kuambukiza katika jamii kwa sababu ya kushindwa kusikiliza maelekezo ya namna ya kujilinda,kujikinga na magonjwa mbalimbali.Pia katika uzalishaji italeta athari nyingi kwa jamii ikiwemo kukosa mazao ya kutosha kutokana na kutosikiliza na kufuata taratibu zinazotolewa na serikali kupitia kwa viongozi.
Kadhalika,Sheikh Isihaka Hassan Salum akitoa mawaidha,aliwasisitizia waumini wa dini ya kiislamu kuishi katika sifa za waumini wa dini hiyo ili kudumisha uhusiano mwema katika jamii ikiwemo Kujichunga na maasi ya kuwaudhi watu na mwenyezi Mungu kwa kuwaudhi watu wengine,kutukana,na kuwanyanyasa.
Pia amesisitiza kuwa muumini bora hapaswi kuwafitinisha watu bali anapaswa kuwaunganisha watu pamoja,wawe na tabia ya kutoweka vitu katika mioyo,bali wawe wepesi wa kusema yanayowaudhi mioyoni mwao na kusamehe ili wakatende mema yale wanayopenda kufanyiwa na wengine.
Akizungumza baada ya swala ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani Rashidi Hakimu,muumini na mkazi wa Mkoa wa Singida amesema leo ni siku njema hivyo ni vema tuisherehekee kwa amani na utulivu na kudumisha tabia njema hasa kimavazi kwa vijana kuendelea kujisitiri kwa vijana hata baada ya mwezi Mtukufu.