Serikali ya mkoa wa Singida
imewaagiza Maafisa Maendeleo wa Halmashauri Saba za mkoa huo kuhakikisha
wanafanya tafiti mbalimbali ambazo zitasaidia wanawake wa mkoa huo ambao
wanafikia Milioni Moja kuanzisha miradi ya kiuchumi itakayowasaidia kujikwamua
na umaskini ikilinganishwa na hali ilivyo kwa sasa.
Mkuu wa mkoa wa Singida Halima
Dendego ametoa kauli hiyo leo (4-Juni-2024)
Mjini Singida wakati azindua Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake la mkoa wa Singida
kiuchumi.
Halima Dendego amesema jukwaa hilo
linatakiwa kuwa na nguvu kuliko majukwaa yote nchini katika kuweka mipango na
mikakati madhubuti ya kuwainua wanawake katika masuala mbalimbali ya kiuchumi
na uongozi.
“Watoeini Wanawake kwenye
mablanketi ya umaskini wasaidieni wainuke kwenye miradi ya kiuchumi
wanayoifanya kwa sababu miradi yao mingi haileti matokeo chanya katika
kubadilisha maisha ya wanawake, Amesisitiza Halima Dendego.
Amesema hatapenda kuona Jukwaa hiyo
linakuwa legelege na kusisitiza kuwa wanawake wengi lazima wajiunge na jukwaa
hilo lenye lengo kubwa la kuwasaidia wanawake kujiimarisha kiuchumi kwa sababu
wapo wengi na uwezo wao.
Mkuu huyo wa mkoa wa Singida
amesema ili kuona Majukwaa hayo ya wanawake yanafanya kazi bila kulala atakuwa
anafanya tathimini ya utendaji kazi kila baada ya miezi Mitatu ili kujua
maendeleo yao na kama kuna changamoto zinazokwamisha maendeleo ya majukwaa hayo zitatuliwe
haraka.
Halima Dendego pia amewahimiza
Wanawake wa mkoa wa Singida kujitokeza kwa wingi bila woga katika kugombea
nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika hivi karibuni
kwa sababu uwezo wa kugombea na kushinda nafasi hizo wanazo kinachotakiwa
kujiamini na kuthubutu.
Naye, Katibu Tawala wa mkoa wa
Singida Dkt. Fatuma Mganga amewataka Maafisa Maendeleo ya jamii katika Halmashauri
Saba za mkoa wa Singida wanakuwa bega kwa bega na wanawake katika kuwashauri na
kuwapatia mbinu mbalimbali za kufanya biashara zenye tija ili kuondokana na
umaskini wa kipato.
Dkt. Fatuma amesema biashara nyingi
wanazofanya baadhi ya wanawake zinaonekana hazina tija hali ambayo inasababisha
baadhi ya biashara zinazoanzishwa kufa kwa sababu hawana elimu ya ujasirimali
na fedha ikiwemo namna ya kukopa kwenye Taasisi za Kifedha ambazo hazina riba
kubwa.
Kwa upande wake, Katibu wa Jukwaa
la Wanawake wa mkoa wa Singida akisoma taarifa ya maendeleo ya Jukwaa hilo
ambalo kwa sasa linafanya kazi katika Halmashauri Tatu za Singida, Ikungi na
Manispaa ya Singida kwa kuwezeshwa na Shirika la UN WOMEN ameomba Serikali
kuendelea kuwasaidia wanawake katika elimu ya ujasiriamali, elimu ya fedha na
uongozi ili waweze kufanya vizuri katika kujiinua kiuchumi katika biashara.
Nao, Wakuu wa Wilaya za Singida na
Ikungi wamemwahidi Mkuu wa mkoa wa Singida kuwa watasimamia kikamilifu maagiza
yake katika kuwasaidia wanawake wa Wilaya zao kuwa bora katika masuala ya
kiuchumi ikilinganishwa na hali ilivyo sasa.
Mkuu wa Wilaya ya Singida Godwin Gondwe, akitoa neno la shukrani kwaniaba ya Mkuu wa Mkoa huo kwa wanachama wa Jukwaa la kuwezesha wanawake kiuchumi la mkoa wa Singida.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Thoams Apson, akizungumza na wanachama wa Jukwaa la kuwezesha wanawake kiuchumi la mkoa wa Singida.
Picha ya pamoja kati ya Mkuu wa mkoa wa Singida na Viongozi
wengine wa mkoa na Viongozi wa Jukwaa la Kuwezesha Wanawake Kiuchumi mara baada
ya kuzindua jukwaa hilo.
No comments:
Post a Comment