SERIKALI imeupatia Mkoa wa Singida Sh.Bilioni 5.8 ambazo zitatumika kujenga vyumba vya madarasa 290 kwa ajili ya wanafunzi watakaojiunga na kidato cha kwanza kuanzia Januari 2023.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, alisema hayo hivi karibuni wakati wa kuwekwa Wakfu Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kati, Askofu Dk. Syprian Hilinti.
Kufuatia hali hiyo, aliwagiza wazazi na walezi kuhakikisha wanafanya maandalizi ya kuwapeleka watoto wao shule watakaoanza darasa la kwanza na wale wa kidato cha kwanza kwani Serikali imeweka mazingira mazuri ya kumuwezesha kila mtoto anapata elimu.
Serukamba ambaye alimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika hafla hiyo, alisena Serikali inatambua na kuthamini mchango wa Kanisa la KKKT katika huduma ya Kiroho na kuhubiri Injili ya amani, umoja, upendo na katika kulea na kukuza vipawa mbalimbali.
"Kanisa la KKKT Dayosisi ya Kati pia linatoa huduma mbalimbali za kijamii kama elimu na afya kwa kushirikiana na Serikali, mfano mmojawapo ni hospitali ya Iambi iliyopo Wilaya ya Mkalama ambayo inamilikiwa na Kanisa hilo ambapo Serikali inalipa mishahara ya watumishi 31 ili kuyawezesha malengo ya Kanisa katika utoaji huduma kwa wananchi," alisema.
Kuhusu kufunguliwa njia ya reli ya kutoka Manyoni kuja Singida, alisena Serikali ya mkoa ilishawasilisha ombi hilo kwa Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa ajili ya kufufua njia hiyo na shirika limeahidi kushughulikia.
Alisema katika suala la ujenzi wa uwanja wa ndege wa kisasa upo katika mpango wa Serikali ambapo mkoa ulipokea maelekezo ya kubainisha eneo ambapo uwanja utajengwa.
Alisema changamoto iliyopo ni kwamba eneo la uwanja wa ndege wa sasa limevamiwa na kujengwa nyumba za makazi jambo ambalo linaunyima sifa uwanja huo kutengenezwa kwa hadhi na kiwango cha kisasa.
"Eneo la pili lililobainishwa na kutengwa Kijiji cha Manga linahitaji malipo makubwa ya fidia ili wananchi waliomo ndani ya eneo hilo wapishe kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa ndege," alisema.
Hata hivyo, alisema suala hilo bado Serikali inaendelea nalo na ana imani jawabu litapatikana kwa ajili ya kufanikisha ujenzi wa uwanja wa ndege wa kisasa hasa kwa kuzingatia jiografia ya Mkoa wa Singida ambao ni jirani ya makao makuu ya nchi.
Kuhusu ujenzi wa barabara ya Singida – Hydom – Mbulu alisema ipo kwenye mpango na utekelezaji wake umeanza ambapo kipande cha Singida – Ilongero – Hydom chenye urefu wa KM 93.3 kazi ya upembuzi yakinifu na maandalizi ya kutangaza zabuni zinaendelea.
Aidha, aliwagiza wakuu wa Wilaya za Singida na Iramba kushughulikia migogoro ya ardhi maeneo ya Kititimo, Ruruma na Ushora na kumpa taarifa ifikapo Novemba 30, mwaka huu ambao Kanisa la KKKT lililalamika kuwa maeneo hayo ambayo ni mali ya Kanisa yamevamiwa.
MWISHO
No comments:
Post a Comment