Katibu Tawala Mkoa wa Singida Mwl. Dorothy Mwaluko leo tarehe 8.11.2022 ametembelea Hospitali, vituo vya Afya na Zahanati vilivyopo Wilaya ya Singida vijijini na Mkalama ili kuona huduma za afya zinavyotolewa katika maeneo hayo.
Akiwa katika ziara
hiyo amekagua Watumishi na utendaji kazi wao vitendea kazi pamoja na usafi wa
mazingira yanayozunguka maeneo hayo.
Dorothy akiwa katika Kituo cha Afya cha Kinyangiri kilichopo
kata ya Kinyangiri Wilayani Mkalama
amewaagiza Waganga wafawidhi katika Hospitali, Zahanati na vituo vya
Afya kusimamia huduma stahiki kwa wagonjwa, maadili ya kazi na utunzaji wa
mazingira ya nje na ndani ya Hospitali ili kuboresha mandhari ya maeneo hayo.
"Nataka mpande miti katika maeneo yenu na pia nataka
kuwe na utaratibu wa upangaji wa vitu Hospitalini (classification) kama ulivyo
utaratibu" alisema Mwaluko
Katibu Tawala huyo akiwa Kinyangiri akamuagiza Mganga Mkuu
wa Mkoa wa Singida Daktari Victorina Ludovick kuhakikisha gari la wagonjwa aina
ya landrova linafanyiwa matengenezo haraka ili liweze kutumika kwa ufanisi
mkubwa.
Hata hivyo Mwaluko akaagiza kuanza kutumika majengo yote
ambayo fedha za umma zimetumika zikiwemo nyumba za wafanyakazi wa sekta ya Afya
kuanza kutumika haraka iwezekavyo.
Aidha ameiagiza timu ya
usimamizi na uendeshaji wa huduma za Afya ya Mkoa huo (RHMT) kuwatembelea watumishi wa Afya mara
kwa mara ili kuwafariji na kuona na kutatua changamoto zinazowakabili.
Naye Mganga mfawidhi wa Kituo cha Kinyangiri Daktari Anna
Kimonga akamueleza Katibu Tawala Mkoa kwamba
Kituo hicho kinapokea Wagonjwa kati
ya 30 mpaka 50 na wanawake wanaojifungua ni kati ya 25 mpaka 30 kwa mwezi
ambapo ameeleza kwamba ni muhimu kuwa na gari la Wagonjwa lenye uwezo wa
kufanya kazi kulingana na mazingira.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Daktari
Dorisila John amesema upatikanaji
wa dawa na vifaa tiba katika Wilaya hiyo unaridhisha huku akibainisha kwamba
kwa mujibu wa muongozo bado Kkna uhitaji wa madaktari na wauguzi katika vituo
vingi vya Afya na Zahanati Wilayani hapo.
Dorisila amesema katika Hospitali ya Wilaya ya Mkalama mpaka
kufikia tarehe 16 Novemba, 2022 ufungaji wa vifaa vya X-Ray utakuwa umekamilika
jambo ambalo wanategemea kwamba huduma za mashine hiyo zitaanza hivi karibuni.
Ziara hiyo ya Katibu Tawala Mkoa wa Singida aliambatana na timu ya usimamizi na uendeshaji wa huduma za Afya Mkoa (RHMT) ambapo walitembelea Zahanati ya Kanisa Katoliki Iguguno, Kituo cha Afya Kinyangiri, Hospitali ya Wilaya ya Mkalama, Hospitali ya rufaa ya Iambi, Hospitali ya Wilaya ya Singida na Kituo cha afya Ilongero.
No comments:
Post a Comment