Maafisa wa Afya na Lishe Mkoani Singida wametakiwa kutembelea mashamba yote ya chumvi yaliyopo Mkoani hapo na kupima chumvi inayovunwa ili kuona kiwango cha Madini joto yaliyomo.
Maagizo hayo yametolewa leo tarehe 11.11.2022 na Katibu
Tawala wa Mkoa huo Mwl. Dorothy Mwaluko alipotembelea mashamba ya chumvi
yaliyopo Sekenke kijiji cha Nkonkirangi Wilaya ya Iramba ili kuona kiwango cha
Madini joto yanayopatikana katika bidhaa hiyo.
Aidha wataalamu wa afya na Lishe walipima chumvi na kubaini
kwamba ina kiwango kidogo cha Madini joto ambapo ndipo Katibu Tawala huyo
alipotoa maelekezo kwa wataalamu hao kuyapitia mashamba yote ya chumvi na
kupima viwango vya Madini joto na
kuwataka kuweka mpango wa kuongezea
Madini hayo kabla ya kumfikia mlaji.
Mwaluko amewataka wataalamu hao kuanza kutoa elimu kwa
wanunuzi wa chumvi hiyo juu ya umuhimu wa madini joto katika mwili wa mwanadamu.
Amesema wanunuzi ndio watakao saidia kuwaelimisha wateja wao
kulingana na bidhaa watakayoihitaji.
Kwa upande wake Kaimu Afisa Lishe wa Mkoa Christowela
Barnaba amesema bidhaa hiyo ni muhimu kuongezewa madini joto ili kuepuka kupata
ugonjwa wa goita jambo ambalo linaweza
kugharimu maisha ya mlaji.
Amesema pamoja na kukutana na wanunuzi wao wataendelea kutoa
elimu kwa wavunaji na wachuuzi pamoja na viwanda kuhakikisha wanauza chumvi
ambayo ina kiwango cha kutosha cha Madini joto.
Naye Afisa Afya wa Mkoa wa Singida Mgeta Sebastiani
amefafanua kwamba mwananchi anahitaji kuwa na afya bora itakayomsaidia
kuzalisha mali na kuongeza kipato na kueleza kwamba ukosefu wa Madini joto inaweza
kusababisha kipato kinachopatikana kutumika kujitibia.
Mgeta amewashauri wavuna chumvi hao kutazama Afya zao kabla ya biashara na kuondoa imani potofu kwamba chumvi ikiongezewa madini joto inabadilika rangi na wateja wataikataa.
No comments:
Post a Comment